TANZANIA KUWA NCHI YA TATU BARANI AFRIKA UZALISHAJI URANI


●Utafiti wabaini akiba ya tani 54,000 za Urani


●Historia inasema kabla ya mwaka 1912 kiasi cha kg 400 za Mbale ya urani zilichimbwa na kusafirishwa


●Uzalishaji utadumu kwa kipindi cha miaka 12 kwa awamu ya kwanza


●Mradi kuvutia uwekezaji wa fedha za kigeni utakaofikia shilingi trilioni 3.6


*Na.Samwel Mtuwa, URANI- Tanzania*


Urani (Uranium) ni elementi ya kemikali yenye alama ya kikemia "U" na namba yake ya atomia ni 92 katika jedwali la elementi. Aidha, Urani ni metali tekevu yenye rangi ya kijivu na nyeupe yenye mionzi ya usumaku.


Kitaalam madini ya Urani mara nyingi huonekana kwa wingi katika mifumo mbalimbali ya madini ambayo ni aina maalum za miamba au maumbo ya kijiolojia kama vile uraninite, pitchblene , carnotite na Autunite.


Tafiti mbalimbali zilizofanyika zimeonesha madini ya Urani nchini Tanzania yaligundulika katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Namtumbo (Mkuju River), Bahi, Galapo, Minjingu, Mbulu,Simanjiro, Ziwa Natroni, Manyoni, Songea ,Tunduru, Madaba , na Nachingwea.


Japokuwa tafiti zinasema kuwa, kabla ya mwaka 1912 kiasi cha kilogramu 400 za mbale ya urani zilichimbwa na kusafirishwa nje ya nchi ambapo toka kipindi hicho hakuna uchimbaji mwingine uliofanyika.


Mradi wa utafiti na uendeshaji wa urani katika eneo la Mkuju River unamilikiwa na kampuni ya Mantra Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Urani ya Urusi (ARMZ) huku kampuni ya Uranium One Inc ndiyo waendeshaji wa mgodi huo.


Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika katika eneo la mgodi wilaya ya Namtumbo mkoani Songea imebainika kuwepo kwa tani 54,000 za urani ambapo kulingana na akiba hiyo uzalishaji utafanyika kwa miaka 12 na kuvutia uwekezaji mkubwa wa fedha za kigeni (FDI) unaofikia zaidi ya shilingi trilioni 3.6.


Tanzania itakapoanza uzalishaji kupitia Mradi wa Mkuju River Wilayani Namtumbo itakuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa madini ya urani baada ya nchi ya Niger yenye akiba ya tani 200,000 na Namibia yenye akiba ya tani 100,000 katika miradi yake mitatu ya uzalishaji.




Nchi ya Niger ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa urani barani Afrika na ni miongoni mwa wazalishaji wakuu duniani.


Uzalishaji wake unafanyika katika migodi mikubwa miwili ambayo ni *Arlit* na *Akouta* inayomilikiwa na kampuni ya Kifaransa Orano zamani ilijulikana kama Areva, ndiyo chanzo kikuu cha urani nchini humo.


Nchi ya Namibia pia ni mzalishaji mkubwa wa urani duniani kupitia migodi yake maarufu ya Rossing Mine inayomilikiwa na Rio Tinto na serikali ya Namibia pamoja na Husab Mine inayomilikiwa na kampuni ya Kichina.


Madini ya urani hutumika katika sehemu mbalimbali ikiwa pamoja na kuzalisha nishati ya umeme, matibabu, na viwandani kutengeneza rangi na glasi kutokana na uwezo wake wa kutoa mionzi.


*Chanzo*



*# Minerogenic Report*

*# Tovuti UraniumOne*

*#AfricaMining.com*

*#TanzaniaInvest.com*

Post a Comment

0 Comments