Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU NA MASLAHI YA JESHI LA POLISI – KATAMBI



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Paschal Patrobas Katambi, amesema Serikali imepanga kuboresha miundombinu ya Jeshi la Polisi kwa kulipatia vitendea kazi bora na vya kisasa pamoja na kuimarisha maslahi ya askari wake.

Katambi ameyasema hayo jana Jumapili katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Zimamoto mjini Shinyanga, wenye lengo la kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa kumchagua tena kuwa mbunge wao.

Amesema Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa ya kulinda raia na mali zao, hali inayowezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa amani na utulivu. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imejipanga kufanya maboresho makubwa ndani ya jeshi hilo kwa kuboresha maslahi ya askari, kuwapatia vitendea kazi vya kisasa na kuimarisha mifumo mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, amewaomba wananchi wa Shinyanga Mjini kuendelea kumuombea mbunge wao, akieleza kuwa majukumu aliyokabidhiwa na Rais ya kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni mazito na yanahitaji ushirikiano pamoja na maombi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amempongeza Katambi kwa rekodi yake nzuri ya utendaji ndani ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi, akisema amekuwa kiongozi anayeiletea heshima Mkoa wa Shinyanga na chama hicho kwa ujumla.

Akijibu baadhi ya hoja na changamoto zilizowasilishwa na wananchi, Waziri Katambi ameahidi kuzishughulikia kwa kadri ya mamlaka yake pamoja na kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya wizara yake kwa ufanisi.

Mkoa wa Shinyanga una wilaya tatu ambazo ni Shinyanga, Kahama na Kishapu, ukiwa na jumla ya majimbo saba ya uchaguzi ambayo ni Shinyanga Mjini, Kahama Mjini, Kishapu, Solwa, Ushetu, Msalala na Itwangi.

Post a Comment

0 Comments