Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza katika Kongamano la wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari lilioandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA TAN)
Na Neema Nkumbi, Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amewataka waandishi wa habari nchini kuitangaza Iringa kama kitovu cha fursa za uwekezaji, akibainisha kuwa mkoa huo umebarikiwa rasilimali nyingi zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akifungua Kongamano la wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari lilioandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA TAN), Machi 17, 2026, RC huyo amesema Iringa ina fursa kubwa katika sekta za kilimo, ufugaji, misitu, viwanda pamoja na utalii, huku akisisitiza kuwa mazingira ya uwekezaji yameboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Amesema sekta ya kilimo inayochangia zaidi ya asilimia 85 ya uchumi wa mkoa huo bado ina nafasi kubwa ya uwekezaji hususan katika umwagiliaji na usindikaji wa mazao, huku uzalishaji wa chakula ukiendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Kwa upande wa viwanda, amesema mkoa una malighafi za kutosha kwa ajili ya uwekezaji katika usindikaji wa mazao ya kilimo, bidhaa za misitu na mifugo, wakati sekta ya utalii ikitajwa kuwa na vivutio vikubwa kama Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Milima ya Udzungwa vinavyoweza kuvutia wawekezaji zaidi.
Aidha, amesema serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara, umeme na usafiri wa anga ili kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, huku maeneo maalum ya ardhi tayari yakitengwa kwa ajili ya wawekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema kongamano hilo linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na wadau wa maendeleo pamoja na kuendeleza uandishi wa habari unaolenga kutoa suluhisho kwa changamoto za jamii.
Soko amesema MISA Tanzania itaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa, huku akiwahimiza waandishi wa habari kuendelea kuandika habari zenye mwelekeo wa suluhisho kwa kuzingatia weledi wao.
Aidha, ameeleza kuwa taasisi hiyo ina mpango wa kuanzisha kituo cha ugawaji wa taarifa za maendeleo kwa jamii, kitakachotoa elimu na taarifa muhimu kwa wananchi, na kuiomba serikali ya mkoa kutoa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amekubali ombi hilo na kueleza kuwa serikali iko tayari kushirikiana na MISA Tanzania kwa kutoa eneo la kujenga kituo hicho cha taarifa.
Naye Meneja wa NSSF Mkoa wa Iringa, Benedict Wela, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwahamasisha Watanzania kujiunga na mfumo wa hifadhi ya jamii ili kujikinga na umaskini na kuwa na usalama wa kipato baada ya kustaafu.





















0 Comments