Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSALALA YAJIPANGA AWAMU YA PILI YA CHANJO YA POLIO, WATOTO ZAIDI YA LAKI MOJA NA SITINI NA SITA KUNUFAIKA

 

Mratibu wa elimu ya afya kwa umma halmashauri ya Msalala Peter Shimba akizungumza na wadau mbalimbali, viongozi wa dini, pamoja na watu mashuhuri katika kikao cha uhamasishaji kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Msalala.



NA NEEMA NKUMBI,MSALALA


Halmashauri ya Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga inatarajia kuanza awamu ya pili ya chanjo ya matone ya polio kuanzia tarehe 7 hadi 10 Mei, 2026, ikilenga kuwafikia zaidi ya watoto laki moja na elfu sitini na sita walio chini ya umri wa miaka kumi.

Akizungumza katika kikao cha uhamasishaji kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo mratibu wa elimu ya afya kwa umma halmashauri ya Msalala Peter Shimba, amesema kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali, viongozi wa dini, pamoja na watu mashuhuri,  amesema chanjo hiyo itatolewa kwa watoto wote kuanzia waliozaliwa leo hadi wenye umri wa miaka tisa na miezi kumi na moja, bila kujali kama walishapata chanjo katika awamu ya kwanza.

Amesema zoezi hilo litatekelezwa kwa njia ya nyumba kwa nyumba, shuleni, masokoni, vituo vya usafiri na maeneo mengine ya mikusanyiko ili kuhakikisha kila mtoto anafikiwa.

“Lengo letu ni kufikia asilimia 100 na zaidi, kama ilivyokuwa awamu ya kwanza ambapo tulivuka lengo na kufikia asilimia 121,” amesema.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uhamasishaji wa Chanjo ya Polio kutoka Wizara ya Afya, Anne Shuma, amesema serikali itahakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo hiyo, huku akionya kuwa hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa kwa wazazi au walezi watakaokwamisha zoezi hilo.

Amesema shule zitatumika kama sehemu muhimu ya kuwafikia watoto wengi, huku ufuatiliaji ukifanyika kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chanjo.

“Hatutegemei wananchi kuwa kikwazo cha kutimiza adhma ya serikali ya kuhakikisha watoto wanapata chanjo ya polio, hivyo tunawaomba wananchi ushirikiano ili kulinda afya ya mtoto,” amesema Shuma.

Naye Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) Mkoa wa Shinyanga, Adelina Apolinary, amesema tayari wamewajengea uwezo wahamasishaji wa jamii (social mobilizers) ili waweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi na kuongeza mwitikio wa chanjo.

Amesema wahamasishaji hao watafanya kazi ya kuwafikia wananchi moja kwa moja, hususan katika maeneo ya vijijini na kwa wale wenye mashaka kuhusu chanjo.

“Tumeendesha mafunzo kwa wahamasishaji wetu ili waweze kutoa elimu na kuondoa hofu au imani potofu kuhusu chanjo,” amesema.

Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), Red Cross, taasisi za kidini, walimu na viongozi wa jamii, huku vyombo vya habari vikitarajiwa kusaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi.

Serikali imeendelea kusisitiza kuwa chanjo ya polio ni salama, haina madhara na ni muhimu katika kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa huo, hivyo wazazi na walezi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo.




Post a Comment

0 Comments