Na Neema Nkumbi, Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amesema ataliwasilisha ombi la wananchi wa mitaa ya Mbulu na Mission la kujengewa shule ya sekondari, baada ya wananchi kueleza changamoto ya umbali wanaotembea wanafunzi kufuata elimu ya sekondari katika shule ya sekondari Nyashimbi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mbulu, Nkinda alisema hoja hiyo ni ya msingi na itafikishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Amesema serikali itafuatilia pia hoja nyingine iliyotolewa na wananchi kuhusu taarifa za uwezekano wa kubadilisha Shule ya Msingi Mbulu kuwa shule ya sekondari, akimsisitiza mwenyekiti wa mtaa kulijadili suala hilo kwa hekma na ushirikishwaji wa wadau kabla ya kufikiwa kwa maamuzi.
Awali, Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Kahama, Masola Juma, alieleza kuwa changamoto ya barabara inayopita Lyanzungu ambapo wanafunzi wanapita sasa inapitika baada ya matengenezo yanayoendelea.
Amesema “Kutokana na maboresho hayo, wanafunzi wanaotumia njia hiyo hawana tena changamoto kubwa ya kupita barabara ya Lyanzungu kama ilivyokuwa awali. Watoto waende shule sasa kwa amani.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mission, Solomon Ruta, ameomba radhi kwa mkuu wa wilaya na wananchi kufuatia malalamiko yaliyotolewa kuhusu utendaji wa ofisi ya serikali ya mtaa, akiahidi kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyobainishwa.
Alisisitiza kuwa uongozi wa mtaa utaendelea kushirikiana na wananchi na viongozi wa serikali, ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati na huduma zinaendelea kuboreshwa.
Mwisho.


0 Comments