Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BANDARI YA DAR ES SALAAM NI LANGO KUU LA BIASHARA NA UCHUMI WA KIKANDA




Bandari ya Dar es Salaam inazidi kuimarika kama lango kuu la kimkakati linalounganisha Afrika na masoko ya dunia, huku ikichochea ukuaji wa uchumi wa kikanda katika kipindi hiki ambacho mabadiliko ya minyororo ya ugavi duniani yanabadilisha mtazamo wa kibiashara.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mashirika Makubwa wa Benki ya Absa Tanzania, Nellyana Mmanyi, wakati akizungumza katika mkutano wa GTR East Africa 2026 uliofanyika jijini Nairobi, Kenya, ukikutanisha wadau wa biashara, fedha, na uwekezaji.

Mmanyi alieleza kuwa mazingira yanayobadilika ya uchumi wa dunia yanaipa Afrika Mashariki fursa ya kipekee ya kuwa kitovu cha uzalishaji na kiunganishi cha kimkakati, akisisitiza kuwa eneo hilo linanufaika na msimamo wake wa kijiografia na uhusiano thabiti na Mashariki ya Kati na Asia.

Alibainisha kuwa bandari hiyo inafanya kazi kubwa ya kuhudumia biashara ya Tanzania pamoja na nchi jirani zisizo na bandari, zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Uganda, na Rwanda, huku Ukanda wa Kati ukiendelea kuimarishwa kama njia kuu na muhimu ya usafirishaji wa mizigo ya kikanda.

Licha ya fursa hizo kubwa, Mmanyi alionya kuwa wafanyabiashara bado wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali vya kuvuka mipaka, ikiwemo ucheleweshaji wa forodha, mifumo isiyo na ufanisi ya usafirishaji, tofauti za kanuni, na changamoto za miundombinu zinazoongeza gharama na muda.

Alisisitiza kuwa ili Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) liwe na tija ya dhati, linapaswa kutoka kwenye ahadi za kisera na kuwa utekelezaji wa vitendo kwa kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru, huku benki zikiendelea kutoa ufadhili jumuishi na huduma za kifedha kusaidia kampuni kukabili changamoto za masoko ya kikanda.

mwisho

Post a Comment

0 Comments