Ujumbe wa wadau wa maendeleo ya elimu ukiwemo Global Partnership for Education (GPE) pamoja na Education Program for Results (EP4R) ukiongozwa na Morten Sigsgaard Mratibu wa Ushirika wa Nchi (GPE) umeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu inayotekelezwa katika Shule ya Msingi na Sekondari Buswelu, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo Mei 11, 2026, Morten amesema miradi hiyo imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hususan kwa wanafunzi wa elimu jumuishi.
Katika Shule ya Msingi Buswelu, inayohudumia wanafunzi 1,211 wakiwemo 176 wenye mahitaji maalumu, imefanikiwa kujenga bweni la wasichana wenye mahitaji maalumu kupitia ufadhili wa Serikali na GPE-LANES II.
Mradi huo9 umewezesha wanafunzi 80 kupata makazi salama ya bweni, huku huduma za bweni zikianza rasmi Mei 8, 2026 baada ya Serikali kuanza kutoa fedha za chakula.
Aidha, walimu na wanafunzi wameeleza mabadiliko chanya yaliyotokana na miradi hiyo, wakisema awali wanafunzi walikuwa wakisoma katika mazingira ya msongamano wa madarasa, lakini sasa wanapata nafasi ya kusoma katika mazingira bora na yenye nafasi ya kutosha, jambo lililoongeza umakini na ushiriki darasani.
Katika Shule ya Sekondari Buswelu, kupitia Programu ya EP4R, shule imepokea Shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vyenye viti na meza 100, mradi ambao tayari umekamilika na unatumika.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanasema awali walikuwa wakisoma wakiwa wamebanana kutokana na upungufu wa madarasa, hali iliyokuwa ikichangia usumbufu wakati wa masomo, lakini kwa sasa wanafurahia kusoma katika madarasa mapya yenye nafasi kubwa na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Uongozi wa shule ulieleza kuwa miradi hiyo imechangia kuboresha ufaulu pamoja na kuongeza hamasa ya kujifunza.
Wadua wa maendeleo walitoa pongezi kwa Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kuboresha mazingira ya kujifunzia nchini.













0 Comments