Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAFUNZO YA PAZA SAUTI+ YAZINDULIWA KAHAMA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI

 

Mratibu wa Mradi wa Paza Sauti + kutoka Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS), Agnes Kirato akielezea mradi wa Paza Sauti leo mei 5, 2026.


Na Neema Nkumbi, Kahama


Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na kwa ufadhili wa Sanlam Allianz, limeanza rasmi mafunzo ya kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia (GBV) na ukatili dhidi ya watoto (VAC) katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Mafunzo hayo yanatekelezwa kupitia Mradi wa Paza Sauti+ unaolenga kuiwezesha jamii kuzungumza wazi dhidi ya vitendo vya ukatili, huku ukijenga uwezo wa watoa huduma za afya katika ukusanyaji na matumizi sahihi ya ushahidi wa kiforensiki.

Kwa mujibu wa ratiba, mafunzo kwa watoa huduma za afya yanafanyika kuanzia Mei 5 hadi 7, 2026, yakifuatiwa na mafunzo kwa Wahudumu wa Afya ya Jamii (CHWs) Mei 8, 2026, Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha utambuzi wa mapema wa matukio ya ukatili, utoaji taarifa sahihi, ukusanyaji wa ushahidi pamoja na utoaji wa huduma bora kwa manusura.

Akizindua rasmi mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Stephen Magalla, amepongeza ushirikiano kati ya THPS, GCLA na Sanlam Allianz akisema ni hatua muhimu katika kukabiliana na ukatili.

“Ushirikiano huu unaakisi mwitikio shirikishi unaohitajika katika kupambana na ukatili wa kijinsia na dhidi ya watoto, Kuimarisha mifumo ya kiforensiki kutaboresha msaada kwa manusura na kuhakikisha wanapata haki kwa wakati,” amesema Magalla.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Sanlam Allianz Life Insurance Tanzania, Julius Magabe, amesema kampuni hiyo imeamua kuunga mkono mradi huo kama sehemu ya mchango wake kwa jamii.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya mradi huu muhimu unaolenga kulinda ustawi na heshima ya jamii, hasa kwa kupambana na ukatili wa kijinsia na dhidi ya watoto,” amesema Magabe.


Mradi wa Paza Sauti+ unalenga kuimarisha uwezo wa kiforensiki, kuhamasisha uripoti wa matukio kwa wakati, kuongeza uelewa wa matumizi ya ushahidi wa vinasaba (DNA) pamoja na kuboresha uratibu kati ya sekta za afya, polisi na ustawi wa jamii.

Mradi huo unatekelezwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama na Kituo cha Afya Nyasubi, ukihusisha kata za Nyasubi na Malunga, ukiendana na Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC II).


Mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni afisa ustawi wa jamii manispaa ya kahama Sesilia Marsel, ameshukuru THPS kwa kuwapatia mafunzo ya namna ya ukusanyaji wa ushahidi pia jinsi ya kuielimisha jamii katika kutunza ushahidi pale ambapo ukatili unatokea maana wazazi wengi hupoteza ushahidi kwa kuwaogesha watoto au kubadilisha nguo kabla ya kufika hospitali.

Naye Daktari kutoka kituo cha afya Nyasubi Abas Dosa amesema mafunzo hayo yatawasaidia kubaini muhusika wa ukatili moja kwa moja ambaye anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa sababu ushahidi wa DNA ni ushahidi usio acha shaka tofauti na zamani ambapo ushaidi ulichukuliwa lakini hakuwa wa uhakika wa mhusika wa ukatili.


Kupitia juhudi hizi, wadau wanaamini kuwa manusura wa ukatili watapata huduma bora kwa wakati, kusikilizwa na hatimaye kupata haki stahiki.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (OC-CID) Kahama, SP Maro Kenyunko, pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii, Abrahamani Kibakaya, ambao walipongeza juhudi hizo kwa kusaidia kuziba mapengo katika kushughulikia vitendo vya ukatili.


Washiriki wa mafunzo hayo ni watoa huduma za afya, maafisa wa dawati la jinsia kutoka Jeshi la Polisi, maafisa ustawi wa jamii pamoja na wadau wa kijamii, wakilenga kuimarisha usimamizi wa kesi kuanzia hatua za awali hadi utoaji wa haki.



TAZAMA PICHA


Post a Comment

0 Comments