Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIKI YA ZIMAMOTO DUNIANI, WANANCHI KAHAMA WAHIMIZWA KUPIGA 114 WAKATI WA DHARURA

 

Mkuu wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari (wa kwanza kulia), akitoa elimu ya utunzaji wa visima vya maji vya zimamoto (fire hydrant), kwa mama lishe na wajasiriamali wa kata ya Nyahanga Manispaa ya Kahama wanaozunguka kisima hicho.


Na mwandishi wetu - Kahama

Jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga limeendelea kutoa elimu ya majanga na maokozi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, katika kuadhimisha wiki ya zimamoto duniani, wilayani humo.




Katika siku ya leo jeshi hilo likiongozwa na mkuu wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga, mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari limetoa elimu ya utunzaji wa visima vya maji vya zimamoto (fire hydrant).




Akizungumza na wananchi wa kata ya Nyasubi mtaa wa Nyakato, Omari amesema lengo la elimu hiyo ni kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika utunzaji wa visima hivyo kwa ajili ya maji ya kuzimamoto wakati wa darura.




Amewataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa visima hivyo, kutokana na baadhi ya watu wasiokuwa waadilifu kuiba mifuniko ya visima.





Askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga SGT Irene Kalula, akikagua mfuniko wa kisima cha maji cha zimamoto (fire hydrant), katika mtaa wa Shunu-Kahama, baada ya jeshi hilo kufanya ukaguzi wa visima hivyo na kuwaeleza wananchi umuhimu wake kwa raia na mali zao. Hii inaambatana na maadhimisho ya wiki ya Zimamoto duniani.




"Kila mmoja awe mlinzi, hivi ni kwa faida yetu sisi endapo yakitokea majanga ya moto kwenye maeneo yetu. Baadhi ya watu wenye nia ovu wanaiba hii mifuniko na kuacha visima wazi." Amesema Omari na kuongeza




"Visima hivi vikiwa wazi ni hatari kwa watoto wetu wanapokuwa wanacheza, lakini pia mtachelewesha utoaji wa huduma endapo litatokea janga la moto kwenye eneo lenu na hii miundombinu ikawa imeharibiwa, tushirikiane na inapotokea dharura yoyote tupigie kwenye nambari 114, tutaitika haraka sana."



Askari wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga FC Mustafa Abdul (kulia), na SGT Irene Kalula, wakitoa elimu kwa wafanyabiashara wa soko kuu - Kahama ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Zimamoto Duniani, wilayani humo.



Pia elimu hii ya majanga na maokozi imetolewa kwa wafanyabiashara wa soko kuu manispaa ya Kahama, wakitakiwa kuepuka mambo yanayoweza kusababisha majanga kwenye maeneo yao, sambamba na kutoa taarifa mapema jeshi la zimamoto pale zinapotokea dharura kwenye maeneo yao.




Amewataka kutoa taarifa za majanga yote yanayohitaji maokozi na sio kwa majanga ya moto pekee ili kurahisisha shughuli za maokozi ya mali na watu pale zinapotokea dharura.




"Unapoona dharura kwenye eneo lako, haraka pika namba 114 huku ukiendelea na hatua za awali. usipambane pekeyako mpaka mwisho unaona umeshindwa ndipo unatutafuta. Piga 114 ng'ombe kaingia kisimani, mtoto, mafuriko, na yale yote yanayohitaji maokozi tutafika."




Akizungumza sokoni hapo askari wa jeshi hilo wilayani Kahama Mustafa Abdul amesema "Tujiepushe kuwa wasababishi wa vyanzo vya moto na majanga mbalimbali kwenye mitaa yetu na maeneo yetu ya biashara. Visima vyetu vya maji tuvifunike, tuwe na tabia ya kukagua mifumo ya umeme kwenye majumba yetu kama tunavyoelekezwa lakini tusijiunganishie umeme kiholela unaweza kusababisha hasara kwenye nyumba yako."




"Nyumba umeijenga kwa miaka sita au saba, inaungua kwa siku moja kwa sababu ya kushindwa kufuata utaratibu unaopewa wa kuunganishiwa umeme, matokeo yake tunasababisha moto, uharibifu wa mali, ulemavu wa kudumu na hata vifo. Tufuate taratibu tujiepushe na majanga haya" Amesisitiza







Askari wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga FC Mustafa Abdul (kulia), akitoa elimu kwa akina mama wauza mbogamboga soko kuu - Kahama ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Zimamoto Duniani, wilayani humo.

Post a Comment

0 Comments