
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, akizungumza na wamiliki wa nyumba za kulala wageni gesti, lodge au nyumba za kupangisha wilayani humo amewasisitika kuwa mgeni yeyote atakayehitaji huduma za kulala au kupangisha lazima awe na Kitambulisho cha Taifa (NIDA), pasipoti ya kusafiria au barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Kijiji au Mtaa.
Na Neema Nkumbi, KAHAMA
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, ameagiza kuanzia sasa mgeni yeyote anayefikia nyumba za kulala wageni, gesti lodge au nyumba za kupangisha wilayani humo lazima awe na Kitambulisho cha Taifa (NIDA), pasipoti ya kusafiria au barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Kijiji au Mtaa, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha ulinzi na usalama na kudhibiti wahalifu wanaoweza kutumia maeneo hayo kujificha.
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wamiliki wa nyumba za kulala wageni na nyumba za kupangisha uliofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Kahama, Nkinda amesema wamiliki wa nyumba hizo wanapaswa kuhakikisha wanawahifadhi wageni waliotambulika pekee, huku wakichukua taarifa zao muhimu ikiwemo majina kamili, namba ya NIDA au pasipoti ya kusafiria na mawasiliano yao.
Dc nkinda amesisitiza kuwa wahudumu wa mapokezi wanapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapobaini kuwa mtu yeyote anayefika hapo mwenye mienendo ya kutia shaka badala ya kumpokea bila uhakiki.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Juma Benjamin, amewataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni kufika katika ofisi za manispaa ya kahama kuchukua vitabu kwa ajili ya kuandikishia wageni huku akiwataka waliohudhuria kuwafikishia wenzao maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha kila mmiliki anatekeleza wajibu wake katika kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.
Naye Kaimu Mkuu wa Kituo cha Polisi Kahama SSP James Luhaja amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Manispaa na wadau wa sekta ya malazi katika kutekeleza mfumo wa ulinzi shirikishi pia amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na vyombo vya dola ni nguzo muhimu ya kuzuia uhalifu, huku akiwataka wamiliki wa lodge kutoa taarifa za haraka wanapobaini mazingira au watu wenye viashiria vya uhalifu.
Katika kuhakikisha utekelezaji wa maagizo hayo unakuwa rahisi, Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Wilaya ya Kahama, Sirieli Richard, amesema mamlaka hiyo imejipanga kupeleka huduma za usajili wa vitambulisho vya taifa katika kata na vijiji vyote vya wilaya hiyo pia amesema ratiba za zoezi hilo zitatangazwa mapema ili wananchi wapate fursa ya kujiandikisha bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.
Sirieli amebainisha kuwa pamoja na ukubwa wa Wilaya ya Kahama na halmashauri zake, hakuna kata wala kijiji kitakachoachwa nyuma katika zoezi la usajili na ugawaji wa vitambulisho ambapo hatua hiyo itawawezesha wananchi wengi zaidi kupata Vitambulisho vya Taifa, jambo litakalorahisisha utekelezaji wa utaratibu mpya wa utambuzi wa wageni katika nyumba za kulala wageni.
Baadhi ya wamiliki wa nyumba za kulala wageni wameeleza kuunga mkono maelekezo hayo, wakisema wamepokea maagizo ya Serikali na wako tayari kuyatekeleza kikamilifu pia wamesema watawahamasisha wahudumu wa mapokezi kuhakikisha kila mgeni anafuata taratibu za utambulisho kabla ya kupatiwa huduma ya malazi, wakiamini hatua hiyo itachangia kudumisha amani na usalama wa Kahama.
Mmoja wa wamiliki hao, Deogratius Joseph, amesema maagizo hayo yatachangia kupunguza uhalifu kwa kuwazuia wahalifu kutumia nyumba za kulala wageni kama maficho, Hata hivyo, ameiomba Serikali kuharakisha utoaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wengi zaidi ili kurahisisha utekelezaji wa utaratibu huo, akieleza kuwa ingawa hatua hizo zinaweza kuathiri biashara kwa muda mfupi lakini manufaa yake katika kuimarisha usalama wa wilaya ni makubwa zaidi.






0 Comments