
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema baadhi ya wanaojihusisha na upotoshaji wa taarifa hawatoi maelezo ya kina kuhusu namna Serikali inavyotumia fedha za ndani kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
Amesema mikopo na hali ya uchumi vinavyozungumzwa mara kwa mara havioneshi picha kamili ya mafanikio ya miradi ya kimkakati inayogharamiwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi.
Msigwa ametaja Mradi wa Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) kuwa mfano, akisema umegharimu shilingi trilioni 6.558.
Amesema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, asilimia 20 ya gharama zilikuwa zimeshalipwa, huku zaidi ya asilimia 80 iliyobaki sawa na zaidi ya shilingi trilioni 5.23 ikilipwa chini ya uongozi wa sasa.
Ameongeza kuwa mradi huo umeongeza uzalishaji wa umeme nchini, ambapo mwaka 2021 uwezo wa gridi ya taifa ulikuwa megawati 1,902, lakini sasa umefikia megawati 4,038, hatua inayozidi mahitaji ya sasa ya matumizi ya umeme nchini.
Kuhusu hitilafu ya umeme iliyotokea Juni 27, 2026, Msigwa amesema ilikuwa changamoto ya kiufundi ya kawaida iliyosababishwa na mifumo ya kujilinda ya mitambo, ambayo ilizima moja kwa moja baada ya kugundua mabadiliko ya hatari kwa usalama wa gridi ya taifa.
0 Comments