Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Vijana 400 Waagwa Kwenda Kufanya Kazi Nje ya Nchi


Na MWANDISHI WETU

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewaaga vijana 400 wa Kitanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuchangia katika Mfuko huo ili kujihakikishia ulinzi wa kijamii na ustawi wa maisha yao ya sasa na baadaye.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga vijana hao, ambao pia walipata elimu ya hifadhi ya jamii kutoka NSSF ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kwa maisha na ajira zao nje ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Sangu alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara unaoendelea kuimarisha diplomasia ya ajira na kufungua fursa salama kwa Watanzania kufanya kazi nje ya nchi, hatua inayoongeza usalama na heshima ya wafanyakazi wa Kitanzania katika soko la ajira la Kimataifa.

Aidha, alisema Serikali inaendelea kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi, hususan vijana na wananchi waliojiajiri, akieleza kuwa Hifadhi Skimu imekuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wananchi na mfumo wa hifadhi ya jamii.

“Nitumie fursa hii kuipongeza Benki ya CRDB na NSSF.Hii ni kazi ya kimkakati kwa mustakabali wa vijana wetu. Zamani walikuwa wakiondoka bila uelewa wa hifadhi ya jamii, lakini sasa kupitia Hifadhi Skimu wanapata elimu na kuelezwa faida za kujiunga na kuchangia, ikiwemo kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu kwao na familia zao,” alisema Waziri Sangu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alimshukuru Waziri Sangu kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya hifadhi ya jamii katika ajenda ya kazi zenye staha, sambamba na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua fursa za ajira ndani na nje ya nchi kwa Watanzania.

Alisema NSSF inaendelea kuboresha huduma zake kupitia mafao mbalimbali, yakiwemo pensheni ya uzee, urithi, ulemavu, uzazi, upotevu wa ajira pamoja na matibabu, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kila mwanachama analindwa katika kila hatua ya maisha yake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Bi. Jane Sorogo, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake unaoendelea kupanua fursa za ajira nje ya nchi kwa Watanzania, pamoja na Waziri Sangu kwa kuhakikisha wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanafuata taratibu sahihi na haki zao zinalindwa.

Alibainisha kuwa mafanikio ya ajira za nje yanategemea ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za umma na sekta binafsi. Aidha, alizishukuru Benki ya CRDB na NSSF kwa kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuwaandikisha vijana hao katika Hifadhi Skimu ili waanze kujiwekea akiba na kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko.


Post a Comment

0 Comments