Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIWANI MHONGOLO: MCHAKATO WA UPATIKANAJI WA EKARI 10 ZA MAKABURI WAENDELEA, MHONGOLO YAPATA KIBALI CHA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI

 


Diwani wa Kata ya Mhongolo katika Manispaa ya Kahama, Mariam Galula, akizungumza na wananchi wa mtaa wa Mbulu kata ya Mhongolo juu ya upatikanaji wa 
ekari 10 kwa ajili ya maziko na kibali cha ujenzi wa sekondari baada ya malalamiko ya wananchi kwa muda mrefu


Na Neema Nkumbi, Kahama




Diwani wa Kata ya Mhongolo katika Manispaa ya Kahama, Mariam Galula, amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kupata eneo la ekari 10 kwa ajili ya makaburi, huku ikiwa tayari imetoa kibali cha ujenzi wa shule mpya ya sekondari itakayohudumia wakazi wa kata hiyo.

Galula ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Mbulu kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi, kutoa mrejesho wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali na kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuzitatua.

Akizungumzia changamoto ya makaburi, Galula amesema suala hilo limekuwa likiwagusa wananchi kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa eneo la kutosha la mazishi, hali inayowalazimu baadhi ya familia kusafirisha miili ya wapendwa wao kwenda maeneo mengine.

Ameeleza kuwa viongozi wamefanya mazungumzo na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA), ambapo eneo la takribani ekari 10 limependekezwa kwa matumizi ya makaburi pia, amesisitiza kuwa mchakato  bado unaendelea na eneo hilo litakabidhiwa rasmi kwa kata.


"Suala la makaburi lilikuwa linaniumiza sana, Tumefanya mazungumzo na mamlaka husika, na mchakato unaendelea. Tunatarajia ukikamilika wananchi wetu watapata eneo la kudumu la mazishi," amesema Galula.

Katika mkutano huo, mwananchi Doto Wilson amewasilisha kero kuhusu ukosefu wa eneo la makaburi, wakieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha gharama kubwa za kusafirisha miili kwenda maeneo ya Sokola na Nyakato kwa ajili ya mazishi pia amehoji baadhi ya tozo zinazohusiana na huduma za mazishi na kuomba ufafanuzi kutoka kwa viongozi.

Kuhusu elimu, wananchi waliiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa shule ya sekondari ndani ya kata hiyo ili kupunguza umbali wanaotembea wanafunzi kwenda Shule ya Sekondari Nyashimbi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbulu, Hamza Shemsa, amesema Serikali tayari imetoa kibali cha ujenzi wa shule mpya ya sekondari itakayohudumia mitaa wa Mbulu.

Amesema kila mtaa utashiriki kujenga madarasa mawili kama mchango wa wananchi, huku Serikali ikitarajiwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu iliyobaki baada ya wananchi kutekeleza sehemu yao.

Aidha, Shemsa ameahidi kuchangia magari kwa ajili ya kusafirisha mawe na vifaa vya ujenzi ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.





Post a Comment

0 Comments