Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI WODI YA WAZAZI NA UPASUAJI KAKOLA



Na Neema Nkumbi, Msalala

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi katika jengo la wodi ya wazazi na huduma za upasuaji katika Kituo cha Afya Kakola, Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Jengo hilo limegharimu zaidi ya Shilingi milioni 269 na linatarajiwa kuongeza uwezo wa kituo hicho kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Kakola na maeneo ya jirani.

Akisoma taarifa ya ujenzi huo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kakola, Dkt. Emanuel Boniface, amesema ujenzi ulianza rasmi Oktoba 2025 na kukamilika Julai 2026.

Amesema Serikali Kuu ilitoa Shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo, huku Halmashauri ya Msalala ikitoa zaidi ya Shilingi milioni 19 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kituo hicho.

“Serikali Kuu ilileta Shilingi milioni 250, na Halmashauri ya Msalala imetoa zaidi ya Shilingi milioni 19 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kituo hiki,” amesema Dkt. Boniface.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema Kituo cha Afya Kakola ni muhimu kwa wananchi kutokana na ongezeko la idadi ya watu katika eneo hilo.

Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Kata ya Kakola ilikuwa na takribani wakazi 51,000, lakini kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakitegemea huduma za zahanati pekee.

“Tunashukuru Serikali Kuu kwa kuleta Shilingi milioni 250 za ujenzi wa jengo hili. Uwepo wa kituo hiki ni hatua muhimu kwa wananchi wa Kakola,” amesema Magangila.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza Halmashauri ya Msalala kwa usimamizi wa ujenzi huo na namna ilivyowasimamia wakandarasi hadi kukamilika kwa jengo hilo.

Mwang’onda amesema jengo hilo limejengwa kwa kiwango kizuri, huku akisisitiza umuhimu wa Halmashauri kuendelea kusimamia kwa karibu miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa.

Post a Comment

0 Comments