Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VATICAN YAPONGEZA TANZANIA KWA USHIRIKIANO NA KANISA

 



Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu, Angelo Accattino ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa karibu na Kanisa Katoliki.


Askofu Mkuu Accattino alisema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Jimbo Katoliki la Mpanda Mkoa wa Katavi.


Alisema ushiriki wa viongozi wa serikali katika shughuli za Kanisa Katoliki ni ishara ya ushirikiano unaolenga kujenga jamii yenye amani na maendeleo.


Kiongozi huyo anayemaliza muda wake nchini alisema ushirikiano huo una umuhimu katika kujenga jamii yenye amani, upendo na mshikamano na akisisitiza umuhimu wa majadiliano ya kidini katika kuimarisha maendeleo ya Taifa.


“Ushiriki wa viongozi wengi kutoka dini mbalimbali na madhehebu yao ni ishara ya madhabahu ya majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi wa jamii yetu,” alisema Askofu Mkuu Accattino.


Alisema maadhimisho ya miaka 25 ya jimbo hilo ni ishara ya kukua kwa imani, mshikamano na ushirikiano kati ya Kanisa, serikali na jamii katika kujenga ustawi wa wananchi.


Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Accattino, mafanikio yaliyopatikana tangu mwaka 2001 ni matokeo ya jitihada za viongozi wa kanisa, waamini na wadau waliojitolea kwa ajili ya maendeleo ya kanisa na jamii.


Alisema katika kipindi hicho, Kanisa Katoliki limeendelea kutekeleza shughuli za kijamii na kiuchumi ukiwemo ujenzi wa vituo vya kilimo na miradi mingine inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.


Askofu Mkuu Accattino alisema Tanzania kwa takribani miaka mitatu na nusu katika utumishi wake imekuwa na kumbukumbu nzuri kwake.

Post a Comment

0 Comments