Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LUKAGA AWAASA WANAFUNZI NYANG’HOLONGO KUJIEPUSHA NA MAKUNDI, MATUMIZI MABAYA YA MITANDAO

Na Paul Kayanda, Mbogwe

MJUMBE wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Pius Zacharia Lukaga, amewataka wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi kujiepusha na makundi yasiyofaa pamoja na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, akisema mwenendo huo unaweza kuchangia kuporomoka kwa maadili miongoni mwa vijana.

Lukaga alitoa kauli hiyo akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya Darasa la Saba yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Nyang’holongo, iliyopo Kata ya Nanda, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.

Aliwataka wanafunzi hao kutumia elimu waliyoipata kujenga maisha yao, huku wakizingatia nidhamu na maadili mema katika jamii.

Alisema matumizi yasiyokuwa na mipaka ya mitandao ya kijamii na kujiingiza katika makundi yasiyofaa ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuwafanya vijana kupoteza mwelekeo wa maisha.

Kutokana na hali hiyo, aliwasisitiza wanafunzi kuwa makini katika kuchagua marafiki pamoja na maudhui wanayofuatilia kwenye mitandao ya kijamii, ili kuepuka athari zinazoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.

Katika hatua nyingine, Lukaga alisaidia kutatua changamoto ya miundombinu iliyowasilishwa na wanafunzi pamoja na uongozi wa shule hiyo, kuhusu uchakavu wa banda linalotumika kupikia uji na chakula kwa wanafunzi.

Lukaga alitoa kiasi cha fedha na kuongoza zoezi la uchangishaji, huku waalikwa wengine wakichangia, na kufanikisha kupatikana kwa zaidi ya Sh milioni 3.2.

Fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa jiko pamoja na stoo ya kuhifadhia vifaa na mahitaji ya chakula shuleni hapo.

Diwani wa Kata ya Nanda, Fikiri William Fante, aliunga mkono juhudi hizo za Lukaga kwa kushiriki katika harakati za kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Fante aliwataka wahusika kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, akieleza kuwa atafuatilia utekelezaji wa mradi huo hadi kukamilika.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyang’holongo, Joseph Gotta, alimshukuru Lukaga pamoja na Diwani Fante, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, kwa juhudi zao za kusaidia shule hiyo kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Gotta aliomba viongozi hao kuendelea kuisaidia shule hiyo, akitaja mahitaji mengine kuwa ni ukarabati wa vyumba vya madarasa pamoja na kukamilishwa kwa jengo ambalo ujenzi wake haujakamilika.

Alisema kukamilishwa kwa miradi hiyo kutasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na hivyo kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora.

Post a Comment

0 Comments