NA NEEMA NKUMBI, MSALALA
WANANCHI wa Kijiji cha Segese Namba 1, Kata ya Segese, Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, wametakiwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti matukio ya uhalifu, ambayo yanaweza kukwamisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa na Diwani wa Kata ya Segese, Patrick Mahona, wakati wa hafla ya kuwaapisha na kuwasimika vijana wa Jeshi la Jadi la Sungusungu, ambapo amesema uwepo wa vitendo vya uhalifu ni miongoni mwa sababu zinazoweza kudumaza maendeleo ya wananchi.
Mahona amesema usalama ni jukumu la kila mwananchi, huku akiahidi kuwa viongozi wataendelea kushirikiana na Jeshi la Jadi la Sungusungu katika kuhakikisha amani na usalama vinaimarika katika eneo hilo.
“Suala la ulinzi ni letu sote. Pale ambapo maendeleo yanakuwepo na uhalifu unaongezeka, naamini hawa vijana watatusaidia, na sisi viongozi tunaahidi kushirikiana nanyi. Hakikisheni mnatekeleza maelekezo ya Sungusungu, maana usalama wa Segese utawakaribisha wawekezaji wengi na kuchangia maendeleo,” amesema Mahona.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kata ya Segese, Mkaguzi Nimrodi Swai, amewataka vijana hao kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na kuyatumia katika kutekeleza majukumu yao ya ulinzi na usalama kwa kuzingatia sheria.
“Niwaombe yale yote mliyofundishwa myashike na kuyazingatia. Hayo ndiyo yatakayokuwa nguzo katika utendaji wenu wa kila siku katika kazi za ulinzi na usalama,” amesema Swai.
Baadhi ya wananchi na wahitimu wa mafunzo hayo wameeleza kuwa Jeshi la Jadi la Sungusungu limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa jamii, hasa katika kukabiliana na matukio ya uhalifu.
Abel Bondo, mmoja wa wananchi wa eneo hilo, amesema Sungusungu imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika kulinda mali na usalama wao.
“Jeshi la Sungusungu kwetu sisi wananchi lina faida kubwa sana. Wahalifu waliwahi kuvamia kwenye kibanda changu usiku, lakini Sungusungu waliwahi kufika. Mimi nilipigiwa tu simu kwamba tayari wamewadhibiti,” amesema Bondo.
Naye mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Ismail Andrea, amesema mafunzo waliyopatiwa yamewajengea uwezo na utayari wa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vya dola katika kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kuwepo katika kijiji hicho.
Jumla ya vijana 240 walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Jadi la Sungusungu katika Kijiji cha Segese Namba 1, ambapo vijana 150 wamefanikiwa kuhitimu mafunzo hayo na kuahidi kushirikiana katika kulinda amani, usalama na mali za wananchi wa kijiji hicho.


0 Comments