Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NKINDA AAGIZA UKUTA UNAODAIWA KUZIBA BARABARA UBOMOLEWE NDANI YA SAA 8



Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Frank Nkinda aliyevaa shati ya pinki na Steven Nyeriga, mwekezaji wa Princessmary English Medium Pre & Primary School ambaye pia ni mtunza hazina wa halmashauri ya Bariadi aliyevaa kofia pamoja na baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Kitwana 

Na Neema Nkumbi, Kahama


Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Frank Nkinda, ameagiza ukuta unaodaiwa kujengwa kwenye eneo la barabara ya wananchi katika Mtaa wa Kitwana, Kata ya Busoka ubomolewe ndani ya saa 8, akisisitiza kuwa hakuna mtu mwenye haki ya kutumia nguvu au uwezo wa kifedha kuwanyima wananchi haki zao kwa kukiuka sheria.


Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo na kusikiliza malalamiko ya wananchi, viongozi wa serikali ya mtaa pamoja na upande unaolalamikiwa, Nkinda amesema serikali haitavumilia vitendo vya kujenga kwenye maeneo ya umma au kuwaondoa wananchi kwenye maeneo wanayodai kuyamiliki bila kufuata taratibu za kisheria.


"Ndani ya saa 8 kuanzia sasa ukuta huo uwe umeondolewa baada ya muda huo kuisha na haujaondolewa, serikali itakuja kuubomoa, Wataalamu wa ardhi waonyeshe mipaka halisi ya barabara ili sheria ifuatwe," amesema Nkinda.


Amesema sheria za nchi zimewekwa kulinda haki za wananchi wote bila kujali uwezo wao wa kifedha, hivyo haitakuwa sahihi kwa mtu yeyote kutumia nguvu au ushawishi kuwabughudhi wananchi.


"Mwenye fedha asitumie uwezo wake kuwaonea wananchi, Wilaya ya Kahama inaongozwa kwa mujibu wa sheria, si kwa ubabe, Migogoro yote ya ardhi lazima itatuliwe kwa kufuata sheria," amesisitiza.


Kauli hiyo imekuja baada ya wananchi kadhaa wa Mtaa wa Kitwana kulalamikia kile walichodai kuwa ni kuzungushiwa ukuta maeneo yao na mwekezaji wa shule ya watoto Princessmary English Medium Pre $ Primary school, jambo walilodai limewazuia kufikia makazi yao na kuhatarisha uwekezaji walioufanya baada ya kununua viwanja hivyo.

Mmoja wa wananchi hao, Yohana Umoja, amesema alinunua kiwanja hicho kwa kufuata taratibu na kujenga nyumba yake kabla ya ukuta wa shule kujengwa ambapo amedai baadaye alikuta uzio umefunga sehemu ya eneo analodai ni lake na kwamba hakuridhishwa na eneo mbadala alilooneshwa.

Naye Emmanuel Godfrey amedai yeye pamoja na wenzake walinunua viwanja hivyo kwa kufuata taratibu za viongozi wa eneo na kupewa nyaraka za umiliki, hivyo wanaamini endapo maeneo hayo yanahitajika kwa matumizi mengine, wanapaswa kufidiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Neema Marwa amesema alitumia miaka mingi kufanya biashara ndogo ndogo ili kujenga nyumba yake na kwamba hayuko tayari kuondoka bila tathmini ya mali yake na makubaliano yanayotambuliwa kisheria.


Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na serikali ya mtaa, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kitwana, Clement Steven, amesema malalamiko yaliyofikishwa ofisini kwake yalihusu zaidi kuzibwa kwa barabara inayotumiwa na wananchi kuelekea kwenye makazi yao.


Amesema tangu mwanzo alimwelekeza mwekezaji kuacha nafasi ya barabara wakati wa ujenzi wa uzio, lakini baadaye ofisi yake ilipokea taarifa kuwa njia hiyo imefungwa, hali iliyosababisha kuitishwa kwa vikao vya viongozi wa mtaa, kata na wataalamu wa ardhi.

Kwa upande wake, Steven Nyeriga, mwekezaji wa Princessmary English Medium Pre & Primary School ambaye pia ni mtunza hazina wa halmashauri ya Bariadi, amesema eneo hilo lina historia ya umiliki inayofahamika, akidai kuwa hakufahamu kama kulikuwa na barabara inayopita katika eneo hilo.

Naye Afisa Ardhi wa Manispaa ya Kahama, Evarist Lameck, amesema Nyeriga anamiliki viwanja namba tatu na namba nne ambavyo ndivyo vilivyopimwa rasmi na kuongeza kuwa endapo alinunua viwanja vingine, alipaswa kuwasilisha nyaraka zake katika Idara ya Ardhi ili vipimwe na kuunganishwa kwa mujibu wa taratibu.

Aidha, Lameck amesema hakuna utaratibu unaoruhusu kufunga barabara ya umma, huku akibainisha kuwa Manispaa ya Kahama haikutoa kibali cha kujenga ukuta huo wa uzio.


Hata hivyo, DC Nkinda amesisitiza kuwa wananchi waliopata maeneo yao kwa kufuata utaratibu hawapaswi kubughudhiwa wala kulazimishwa kuondoka kabla ya sheria kufuatwa.


"Hawa wananchi hawakuiba maeneo haya wamenunua kwa mujibu wa taratibu, Kama kuna anayehitaji eneo lao, sheria ifuatwe, Hakuna atakayelazimishwa kuondoka kwa nguvu," amesema.


Ameongeza kuwa iwapo uchunguzi wa wataalamu wa ardhi utabaini kuwa upande wowote umevamia eneo la barabara au umejenga kinyume cha sheria, hatua za kisheria zitachukuliwa bila upendeleo.
 
"Tukibaini kuna aliyejenga ndani ya barabara, hatua zitachukuliwa bila kujali ni nani, Serikali itasimamia haki kwa kila upande," amesema.

Maagizo hayo sasa yanasubiri utekelezaji huku wananchi wakitarajia uchunguzi wa wataalamu wa ardhi kubaini mipaka halisi ya eneo linalobishaniwa na kutoa suluhu ya kudumu kwa mgogoro huo. 




Post a Comment

0 Comments